Monday, April 9, 2018

MAPENZI NAWE SIWEZI

Kigugumizi natoa, kiloniziba midomo.
Kama bwege nilikuwa,sasa naweka mgomo.
Nakwambia bila dowa, tena nina msimamo.
Mapenzi nawe siwezi, nimechoka kudanganywa.


Waitesa roho yangu, unitoe nikazimu.
Sana kukupenda kwangu, Leo imekuwa sumu.
Nalia na moyo Wangu waanza kuvuja damu.
Nimechoka kudanganywa, mapenzi nawe siwezi.


Waimba kuku alale, eti kipanga yu aja.
Babaisha mwanakele, mzuri kutoa hoja.
Tena wapaza kelele, nisamehe hili moja.
Nimechoka kudanganywa, mapenzi nawe siwezi.


Sitokujali kimwana, leo penzi nalivua.
Mbele yako nakukana, mrembo sojitambua.
Japo macho yasonona, moyo ndo umeamua. Mapenzi nawe siwezi, nimechoka kudanganywa.

Kweli kupenda maradhi, nasadiki walonena.
Sikukupenda baadhi, nilikupenda kwa kina.
Leo ninamwaga radhi, kwaheri tutaonana.
Mapenzi nawe siwezi, nimechoka kudanganywa.


Sina kinyongo na wewe, kwa kuwa tumeachana.
Nakuomba jitambuwe, kwa tabia hujafana.
Uzuri ujirembue, ninakwambia bayana.
Nimechoka kudanganywa, mapenzi nawe siwezi.



_*BY BIN HAMZA*_

_*OCHU*_

_*Mfungwa huru*_
๐Ÿ’ž    MSUSI   ๐Ÿ’ž

Swali sio tashtiti, nawauliza jamani.
Kwa lugha iso masharti, nyepesi pia laini.
Nawauliza banati, na wavulana kundini.
NINI ANACHOKISUKA?, MSUSI HUYU JAMANI.

Msusi wa khairati, mamboye si ya kihuni.
Hazikamati njukuti, kuziweka mapajani.
Wala hasuki makuti, yanoezekwa paani.
NINI ANACHOKISUKA?, MSUSI HUYU JAMANI.

Ukili haukamati, hasubutu asilani.
Mikeka na mabusati, si fundi wa hii fani.
Nywele zao mabanati, hazitii mikononi.
NINI ANACHOKISUKA?, MSUSI HUYU JAMANI.

Maarufu kama nyati, wa hapa kwetu mbugani.
Sifaze hazipatiki, kwengineko duniani.
Wala sio afiriti, wakufanya kila fani.
NINI ANACHOKISUKA?, MSUSI HUYU JAMANI.

Si msusi atiati, atangetange njiani.
Madema hayana chati, masusu hayatamani.
Hayasuki abadati, 
Kwake hayana thamani.
NINI ANACHOKISUKA?, MSUSI HUYU JAMANI.

Jimwage ingila kati, utoe yako maoni.
Zawadi ya biskuti, nitakupa kwa yakini.
Utujibu kwa udhati, tukijue hadharani.
NINI ANACHOKISUKA?, MSUSI HUYU JAMANI.


๐Ÿค—By ochu๐Ÿค—

๐ŸŒท Free    prisoner๐ŸŒท
*_KOMAMANGA_*

Naja tena himahima, kuyajuza ya moyoni.
Yanayonitia homa, kunikondesha mwilini.
Wala bado sijakoma, japo nipo taabani.
Tungo ya leo matata, komamanga lake jina.


Hili tunda la ajabu, nikiliona machoni.
Laitoa yangu hubu, kuliona sitamani.
Tena linananipa tabu, kichefuchefu moyoni.
Komamanga sio shani, lachafua  moyo wangu.

Njiani ninapopita, nikiliona mtini.
Kasoroze huzipata, nyingi zisizo kifani.
Komamanga kulipata, na kuchuma sitamani.
Kwangu halijawa jema, silitaki komamanga.


Tunda kwenu maarufu, nasaba yake peponi.
La huku nalikashifu, lapasuka li mtini.
Nje likiwa nadhifu, mafunza tele kwa ndani.
Sitamani komamanga, Lachafua moyo wangu.


Ladha yake mbaya sana, yakirihisha rohoni.
Chunguchungu utaona, ukafu ndo namba wani.
Utamu wala halina, chapwa chapwa mdomoni.
Komamanga silitaki, kula hata sitamani.


Kwa mimi nasema wazi, bora libaki mtini.
Wala sitaitwa mwizi, litaozea mtini.
Kulichuma Kwangu kazi, komamanga sitamani.
Sitochuma sitokula, komamanga silitaki.


_*by mfungwa huru*_
๐Ÿ—ฃ_*CHAFYA!!!*_ ๐Ÿ—ฃ

Nimechoka kuibana, chafya leo naitoa.
Domo langu liwa pana, vimate tawarushia.
Naacha kubanabana, nimeshindwa izuia.
Nimechoka kuibana, chafya leo naitoa.

Inanichachafya sana, nimeshindwa vumilia.
Pindipo nikiibana, huwenda nikajifia.
Leo ndio nikaona,  hadharani kuitoa.
Nimechoka kuibana, chafya leo naitoa.


Chafya! chafya! naiona, wengi itawaumbua.
Chafya siitoi kona, uwanjani naitoa.
Sijali zenu fitina, maneno 'shayazoea.
Nimechoka kuibana, chafya leo naitoa.


Kinywa changu ni kipana, cha mamba fananishia.
Na meno yamepangana, makali kurarulia.
Nyuwazi yameachana, cheche ndimo hupenyea.
Nimechoka kuibana, chafya leo naitoa.


Vimate vikikutana, usoni kukurukia.
Harufuye mbaya sana, uso utajivimbia.
Chafya ya kimasikina, ugonjwa itakutia.
Nimechoka kuibana, chafya leo naitoa.


Chafya nikitulizana, nikiogopa kutoa.
Mashaka yatanibana, na mengine ya dunia.
Chafya! Chafya! nitapona, zitapungua ghasia.
Nimeshindwa kuibana, chafya leo naitoa.


_*BY OCHU*_

_*mfungwa huru*_
_*NILIPOKUFATA*_

Moyo wangu ulidunda, mwanzo nilipokufata.
Nilizani utakwenda, pale nilipokuita.
Kwani ulikuwa nyonda, sura yako sinyorita.
_*Moyo wangu ulidunda, mwanzo nilipokufata.*_


Nilikuona mcheshi, mwenye tabasam pia.
Sikukwambia uzushi, yale yanonisumbua.
Nawe hukuwa m-bishi jibu zuri ukatoa.
_*Moyo wangu ulidunda, mwanzo nilipokufata.*_


Moyo wangu ulipenya, kwenye zote chemba zako.
Na wewe uliniponya, kwa zuri lako tamko.
Niliruka kama panya, kwa furaha na kicheko.
_*Moyo wangu ulidunda, mwanzo nilipokufata.*_


Nakupenda peke yako, hili halina utata.
Nikikosa pendo lako, duniani nitajuta.
Nipende bila vituko, waseme wanaobwata.
_*Moyo wangu ulidunda, mwanzo nilipokufata.*_


*_by Ochu-mimi_*

_*Mfungwa huru*_
_*KIMWANA UMENIWEZA*_

Acha leo niyanene,  maneno kukuambia.
Midomo nisiibane, utumu menikolea.
Moyo Uwachwe sonone, wazi nakumtamkia.
Kwa kweli umeniweza, penzi limenikolea.


Mitego yako sikane, mpenzi wanijulia.
Lengo lako unibane,  nisije kukukimbia.
Menifanya nisione, kipofu kwako tambua.
Kikweli umeniweza, penzi limenikolea.


Sijui kipi ninene, Utamu menizidia.
Pasua moyo uone, peke yako umekaa.
Njoo basi nikukune, penzi lizidi kumea.
Kimwana umeniweza, kukuwacha sijawaza .


_*Mfungwa huru*_
_*KIINI MACHO*_


itatufika hasara, tukiwa twayapuuza.
Tupaparike papara, kabla kuingia kiza.
Kiona miji yang'ara, ujuwe waning'ariza.
Tutabaki kushangaa, mazuri ughaibini.


Kiini macho wabunge, mawaziri natuhumu.
Twanyanyasika wanyonge, kwetu maisha magumu.
Wanazila zetu tonge, wamenogewa utamu.
Tutabaki tu kuimba, maisha bora nchini.


Sheria kwetu WA chini, ndio tuliotungiwa.
Walo juu kiririni, kiwabana hupinduwa.
Kiini macho machoni, hivihivi twaibiwa.
Tutabaki tu kuimba, sote chini ya sheria.


Si kesi mahakamani, mfungwa huru najua.
Mengi huwa natamani, ndo mana nayasemea.
Hongo zao kibindoni, ndizo zinotununua.
Tutabaki tu kuimba, rushwa adui wa haki.



_*Mfungwa huru*_
_*MAMLAKA YA WACHACHE*_


Nchi giza la ajabu, tena yatoa viroja.
Si bibi wala mababu, wote wanatoa hoja.
Kwamba linawaadhibu, kila mtu aporoja.
Ukenda kwao khatibu, jibu lao huwa moja.
Daraka ni mamlaka, ya wachache kutumbua.


Darakani Kuna kutu, kutu zisosugulika.
Kwani mamlaka watu, watu wasonadhifika.
Tena huwa watukutu, watukutu kwa hakika.
Wala hawanao utu, utu kwao metoweka.
Daraka ni mamlaka, ya wachache kutumbua.


Voti huenda kupiga, viongozi kuchagua.
Tena hugeuka twiga, shingo refu twainua.
Hukaa myayo twapiga, bila ya kujali njaa.
Viongozi watupiga, baada kuwachagua.
Daraka ni mamlaka,  ya wachache kutumbua.


Wakishapata daraka, hutanua zao pawa.
Hujiona wafurika, kwa mali ndo huchagawa.
Kumbe huja poromoka, kwa kiasi hupagawa.
Ni kazi yake rabuka, kwa kiburi 'lichotaoa.
Daraka ni mamlaka,ya wachache kutumbua.


Mwisho nawapa usia, walowepo darakani.
Dunia ni kama njia, tenda wema darakani.
Haki kwetu kuzitoa, ili tuwe afuweni.
Mungu atakujazia, akhera na duniani.
Daraka ni mamlaka,  ya wachache kutumbua.


2015 at L.S.S


_*By Ochu*_

_*Mfungwa huru*_
*_UKALI WAKE PORINI_*๐Ÿ†๐Ÿ†


Kuna mapori sahali, katika mbuga na nyika.
Yaliyojitenga mbali, kisehemu na mipaka.
Muna wanyama wakali, na wanaoyayatika.
Ukali wake porini, vinyama vyasulubika.


Simba dume mfalume, katika pori la taza.
Wala hanacho kimeme, njaa inapomkwaza.
Mbioze Kama umeme, paa swala hufukuza.
Ukali wake porini, vinyama vyasulubika.


Pori la zaza nakama, iliwapata zamani.
Maji wanaita mma, malkia kawa duni.
Inapokuja neema, Simba dume huja ndani.
Ukali wake porini, vinyama vyasulubika.


Sautile kama radi, chini inapoanguka.
Vitimbi na zake kedi, vinyama vinasumbuka.
Ubaya zake hasadi, malkia kamchoka.
Ukali wake porini,  vinyama vyasulubika.


Kukimbia hawawezi, digidigi nyani pia.
Wanamuomba mwenyezi, shufaa kuwapatia.
Simba dume kawa chizi, kutwa anawavamia.
Ukali wake porini, vinyama vyasulubika.



BY OCHU

_*MFUNGWA HURU*_
***MWALIMU***
1)Kilio changu natoa, sikieni nyi kaumu. Hakuna wakukosoa, nayasema mufahamu. Si dibeti nawambia, na mdahalo haramu. Mwalimu athaminiwe, hadhiye iyonekane.
2)Jukumule mwatambua, akifika skulini, darasani huingia, vipindivye kwa foleni, mwili umejichokea anaporudi nyumbani. Huruma namuonea,
hali yake taabani.
3) Arudiapo nyumbani, bado huwa yu kazini. huziandaa lesani, japo nyinyi hamuoni. kweli yuko mashakani, kitanda hakitamani.  athaminiwe mwalimu, hadhiye iyonekane.

4)Mwalimu yeye ndo chanzo, maendeleo nchini. mwalimu ndie kigezo, kwa walio darakani. yeye kawapa mafunzo, walipokua shuleni. Mwalimu athaminiwe, hadhiye iyonekane
5)Mafunzo
mzo kwa mzo, walipatiwa yakini. daktari acha bezo,injinia kaa chini. vikosi siwe gumzo, mwalimu mkamuhini.bila yeye asilani, musengefika mulipo.
6) mshahara wake duni, laki mbili thamanini. hununulia sabuni, chakula hakuna ndani, tarehe pili mwezini, anakopa kwa jirani. mwalimu athaminiwe hadhiye iyonekane.


   Mfungwa huru
TUNAKWENDA MRAMA

Chombo chaenda mrama, angalieni
Tulipotoka,tulipo na tuendako
Kina cha maji chapanda.


Na nahodha akasema, takulindeni, tutaokoka, katika misukosuko , pasi na tanga kutanda.


Tunasonga ma!ma!ma!ma!, mkondoni,
Tunateseka, nahodha toa tamko,
'Tafika tunapokwenda.


Tunakwenda mrama, tuunganeni,
Kunusurika, katika mahangaiko,
Tufike tunakokwenda.


Nahodha huyu si mwema, tumsuteni,
Mwema kuweka, asio na chokochoko,
Afueni itatanda.


By ochu



Mfungwa huru
_*MAWAZO*_

Asubuhi na mapema, naamka nikiwaza.
Kwamba lini nitasoma, niondokane na kiza.
Nikapatwa na muhuma, kwa sana kuwazawaza.
Mawazo ya akili, fakiri ndipo utende.


Siku nyengine hawaza, wapi tapata elimu?.
Nikaenda kuuliza, nikambiwa mwendazimu.
Mbele kukatanda kiza, kanitoka yangu hamu.
Mawazo ya akilini, fakiri ndipo utende.


Siku nenda siku rudi, wazo langu hurejea.
Nikaifanya juhudi, elimu 'jitafutia.
Nikamuomba wadudi, kweli kanisaidia.
Mawazo ya akilini, yanaweza kuwa sawa.


Nikaipata elimu, ya akhera na dunia.
Sasa naitwa mwalimu, kwa wazo lofikiria.
Kumbe mawazo matamu, yale yalio sawia.
Mawazo ya akilini, mengine huwa mazuri.


Kuna mawazo mabaya, mengine hujitokeza.
Hukupeleka kubaya, hukugubika na kiza.
Jiepushe hima haya, uepuke hiyo adha.
Mawazo ya akilini, kuwaza na kuwazua.


_*Mfungwa huru*_
_*UMOJA*_

Wahenga walichonena, umoja huwa ni nguvu.
Na walileta maana, umoja sio uchovu.
Sasa wengi wamenuna, wamevimbwa na mashavu.
Umoja nguvu daima, ikiwa mutapatana.


Mali huzichuma wote, wakubwa wadogo pia.
Si lolote si chochote, wadogo wadhulumiwa.
Pia bado waufyate, bila ya kujitetea.
Umoja nguvu daima, ikiwa mutapatana.


Usikubali dhuluma, mola ametuambia.
Jiepushe himahima, dhulumiwa dhulumia.
Wala usikate tama, chako halali pania.
Umoja nguvu daima, ikiwa mutapatana.


Mukiwa na moja lengo, dhamira na moja nia.
Mukaipanga mipango, mbali mutajifikia.
Mutakwenda songombingo, pale mukijibagua.
Umoja nguvu daima, ikiwa mutapatana.


Ukiwa u umojani, hasara itatufika.
Ila ukiwa makini, utabaki nufaika.
Huu si wa Marekani, ni wa hapa Afirika.
Umoja nguvu daima, ikiwa mutapatana.


_*Mfungwa huru*_