Monday, April 9, 2018

🗣_*CHAFYA!!!*_ 🗣

Nimechoka kuibana, chafya leo naitoa.
Domo langu liwa pana, vimate tawarushia.
Naacha kubanabana, nimeshindwa izuia.
Nimechoka kuibana, chafya leo naitoa.

Inanichachafya sana, nimeshindwa vumilia.
Pindipo nikiibana, huwenda nikajifia.
Leo ndio nikaona,  hadharani kuitoa.
Nimechoka kuibana, chafya leo naitoa.


Chafya! chafya! naiona, wengi itawaumbua.
Chafya siitoi kona, uwanjani naitoa.
Sijali zenu fitina, maneno 'shayazoea.
Nimechoka kuibana, chafya leo naitoa.


Kinywa changu ni kipana, cha mamba fananishia.
Na meno yamepangana, makali kurarulia.
Nyuwazi yameachana, cheche ndimo hupenyea.
Nimechoka kuibana, chafya leo naitoa.


Vimate vikikutana, usoni kukurukia.
Harufuye mbaya sana, uso utajivimbia.
Chafya ya kimasikina, ugonjwa itakutia.
Nimechoka kuibana, chafya leo naitoa.


Chafya nikitulizana, nikiogopa kutoa.
Mashaka yatanibana, na mengine ya dunia.
Chafya! Chafya! nitapona, zitapungua ghasia.
Nimeshindwa kuibana, chafya leo naitoa.


_*BY OCHU*_

_*mfungwa huru*_

No comments:

Post a Comment