Monday, April 9, 2018

*_KOMAMANGA_*

Naja tena himahima, kuyajuza ya moyoni.
Yanayonitia homa, kunikondesha mwilini.
Wala bado sijakoma, japo nipo taabani.
Tungo ya leo matata, komamanga lake jina.


Hili tunda la ajabu, nikiliona machoni.
Laitoa yangu hubu, kuliona sitamani.
Tena linananipa tabu, kichefuchefu moyoni.
Komamanga sio shani, lachafua  moyo wangu.

Njiani ninapopita, nikiliona mtini.
Kasoroze huzipata, nyingi zisizo kifani.
Komamanga kulipata, na kuchuma sitamani.
Kwangu halijawa jema, silitaki komamanga.


Tunda kwenu maarufu, nasaba yake peponi.
La huku nalikashifu, lapasuka li mtini.
Nje likiwa nadhifu, mafunza tele kwa ndani.
Sitamani komamanga, Lachafua moyo wangu.


Ladha yake mbaya sana, yakirihisha rohoni.
Chunguchungu utaona, ukafu ndo namba wani.
Utamu wala halina, chapwa chapwa mdomoni.
Komamanga silitaki, kula hata sitamani.


Kwa mimi nasema wazi, bora libaki mtini.
Wala sitaitwa mwizi, litaozea mtini.
Kulichuma Kwangu kazi, komamanga sitamani.
Sitochuma sitokula, komamanga silitaki.


_*by mfungwa huru*_

No comments:

Post a Comment