_*MAMLAKA YA WACHACHE*_
Nchi giza la ajabu, tena yatoa viroja.
Si bibi wala mababu, wote wanatoa hoja.
Kwamba linawaadhibu, kila mtu aporoja.
Ukenda kwao khatibu, jibu lao huwa moja.
Daraka ni mamlaka, ya wachache kutumbua.
Darakani Kuna kutu, kutu zisosugulika.
Kwani mamlaka watu, watu wasonadhifika.
Tena huwa watukutu, watukutu kwa hakika.
Wala hawanao utu, utu kwao metoweka.
Daraka ni mamlaka, ya wachache kutumbua.
Voti huenda kupiga, viongozi kuchagua.
Tena hugeuka twiga, shingo refu twainua.
Hukaa myayo twapiga, bila ya kujali njaa.
Viongozi watupiga, baada kuwachagua.
Daraka ni mamlaka, ya wachache kutumbua.
Wakishapata daraka, hutanua zao pawa.
Hujiona wafurika, kwa mali ndo huchagawa.
Kumbe huja poromoka, kwa kiasi hupagawa.
Ni kazi yake rabuka, kwa kiburi 'lichotaoa.
Daraka ni mamlaka,ya wachache kutumbua.
Mwisho nawapa usia, walowepo darakani.
Dunia ni kama njia, tenda wema darakani.
Haki kwetu kuzitoa, ili tuwe afuweni.
Mungu atakujazia, akhera na duniani.
Daraka ni mamlaka, ya wachache kutumbua.
2015 at L.S.S
_*By Ochu*_
_*Mfungwa huru*_
No comments:
Post a Comment