Monday, April 9, 2018

MAPENZI NAWE SIWEZI

Kigugumizi natoa, kiloniziba midomo.
Kama bwege nilikuwa,sasa naweka mgomo.
Nakwambia bila dowa, tena nina msimamo.
Mapenzi nawe siwezi, nimechoka kudanganywa.


Waitesa roho yangu, unitoe nikazimu.
Sana kukupenda kwangu, Leo imekuwa sumu.
Nalia na moyo Wangu waanza kuvuja damu.
Nimechoka kudanganywa, mapenzi nawe siwezi.


Waimba kuku alale, eti kipanga yu aja.
Babaisha mwanakele, mzuri kutoa hoja.
Tena wapaza kelele, nisamehe hili moja.
Nimechoka kudanganywa, mapenzi nawe siwezi.


Sitokujali kimwana, leo penzi nalivua.
Mbele yako nakukana, mrembo sojitambua.
Japo macho yasonona, moyo ndo umeamua. Mapenzi nawe siwezi, nimechoka kudanganywa.

Kweli kupenda maradhi, nasadiki walonena.
Sikukupenda baadhi, nilikupenda kwa kina.
Leo ninamwaga radhi, kwaheri tutaonana.
Mapenzi nawe siwezi, nimechoka kudanganywa.


Sina kinyongo na wewe, kwa kuwa tumeachana.
Nakuomba jitambuwe, kwa tabia hujafana.
Uzuri ujirembue, ninakwambia bayana.
Nimechoka kudanganywa, mapenzi nawe siwezi.



_*BY BIN HAMZA*_

_*OCHU*_

_*Mfungwa huru*_

No comments:

Post a Comment