💞 MSUSI 💞
Swali sio tashtiti, nawauliza jamani.
Kwa lugha iso masharti, nyepesi pia laini.
Nawauliza banati, na wavulana kundini.
NINI ANACHOKISUKA?, MSUSI HUYU JAMANI.
Msusi wa khairati, mamboye si ya kihuni.
Hazikamati njukuti, kuziweka mapajani.
Wala hasuki makuti, yanoezekwa paani.
NINI ANACHOKISUKA?, MSUSI HUYU JAMANI.
Ukili haukamati, hasubutu asilani.
Mikeka na mabusati, si fundi wa hii fani.
Nywele zao mabanati, hazitii mikononi.
NINI ANACHOKISUKA?, MSUSI HUYU JAMANI.
Maarufu kama nyati, wa hapa kwetu mbugani.
Sifaze hazipatiki, kwengineko duniani.
Wala sio afiriti, wakufanya kila fani.
NINI ANACHOKISUKA?, MSUSI HUYU JAMANI.
Si msusi atiati, atangetange njiani.
Madema hayana chati, masusu hayatamani.
Hayasuki abadati,
Kwake hayana thamani.
NINI ANACHOKISUKA?, MSUSI HUYU JAMANI.
Jimwage ingila kati, utoe yako maoni.
Zawadi ya biskuti, nitakupa kwa yakini.
Utujibu kwa udhati, tukijue hadharani.
NINI ANACHOKISUKA?, MSUSI HUYU JAMANI.
🤗By ochu🤗
🌷 Free prisoner🌷
No comments:
Post a Comment