Sunday, October 11, 2020

Ndimi Zenye Ncha

DIWANI YA NDIMI ZENYE NCHA

Katika zama ambazo, watu zama hizo hudhani kwamba Ushairi wa Kiswahili ni Tasnia inayowahusu watu wa kale au kwa lugha nyepesi wazee,  na kamwe hauna nafasi, faida wala hadhi kwa vijana wa sasa.

Ni katika zama ambazo, watu wa zama hizo wamegubikwa na fikra za kwamba Ushairi wa Kiswahili katu hauna nafasi kwa watu wenye elimu za madaraja ya juu, ni kazi ambayo hufanywa na watu wasio na elimu pekee.

Ni katika zama ambazo, watu wa zama hizo wamegubikwa na fikra za kwamba Ushairi wa Kiswahili ni Tasnia ambayo inapaswa kushughulikiwa na watu wa jinsia ya kiume pekee na kuwafanya wanawake kwamba hawana nafasi katika Tasnia hii.

Ni katika zama ambazo, watu wa zama hizo mawazo na fikra zao hudhani kwamba ushairi wa Kiswahili ni Tasnia ya kipuuzi ambayo hushughulikiwa na watu wasio na ujuzi wala kazi yoyote ya kitaalamu, bali ni watu wa maskani na vijiweni pekee ndio watu halali wa tasnia hii ya Ushairi.

Ni katika zama ambazo, watu wa zama hizo  hudhani ya kwamba kazi kubwa ya Ushairi wa Kiswahili ni Tasnia inayoeleza ujumbe wa kimapenzi tu, hivyo wanaopaswa kushughulikia na watu fulani ambao fikra zao zaidi zimejikita katika mambo ya mapenzi na si vyenginevyo.

Ni katika zama ambazo, watu wa zama hizo hawana fikra za kwamba Ushairi wa Kiswahili unaweza kuwaunganisha watu wa maeneo mbali mbali ya nchi ya na kuwaweka sehemu moja.

Basi katika zama hizo hizo, ndipo mimi na wenzangu wa rika tafauti wakiwemo vijana wadogo, wazee, wanaume na wanawake wakaamuwa kukaa sako kwa bako, wakashikana mikono, wakaongozana hatuwa kwa hatuwa na kuamuwa kuziunganisha ndimi zao kwa pamoja zikawa ni “Ndimi Zenye Ncha”, tena zenye ncha kali, na kuamua kuziuwa na kuzizika fikra potofu na hasi za watu za zama waufikirio Ushairi tafauti na uhalisia wake.

Diwani ya Ndimi Zenye Ncha ni juhudi zetu Wasanii 34, ambao nia na dhamira ni kufikisha ujumbe kwa jamii kupitia Tasnia hii, walikaa pamoja, wakatafakari na kuamua kwa pamoja kutoa Diwani hii, kwa minajili ya kuvirithisha vizazi vilivyopo katika zama hizi na vile vya zama zijavyo Tasnia hii inayosemwa ndio Tasnia kongwe katika Kazi za Fasihi, huku wakikubaliana na msemo usemao “Nchi isio thamini Ushairi wake, basi nchi hio haina urithi” na wengine husema “Nchi isiyo na Washairi basi watu wa nchi hio ni sawa sawa na wafu”. 

 Washiriki wa Diwani hii ni watu wa umri na rika tafauti, humu kuna vijana wadogo ambao kama si maadili mema waliyoyapata kwa wazazi na jamii yao basi si hasha ukawakuta wakivaa milegezo na sarawili zilizochanwa chanwa mapajani na magotini, ili kudhihirisha ubarobaro na ujana wao, lakini kizuwizi cha maadili waliyokuzwa nayo ndicho kilichawafanya wasivae vivazi kama hivyo, pia wamo watu wa rika la kati kama langu sambamba na wazee wenye wajukuu, uwemo wao unaashiria kwamba kumbe Ushairi wa Kiswahili ni Tasnia ya watu wa rika zote.

Diwani hii pia ina washiriki wenye Elimu za Madaraja tafauti, kuna washiriki ambao hawakubahatika kupata elimu kabisa, kuna wenye elimu za wastani na kuna washiriki wenye elimu za ngazi ya Cheti, Stashahada, Shahada, shahada ya Uzamili na Shahada ya Uzamivu, tena wakiwemo wenye shahada za Uhasibu. Shahada za Uongozi, Shahada za Uwakili, Shahada za Nyukilia na Mionzi na nyenginezo, hii inaonesha dhahiri kwamba, kumbe Ushairi unawagusa watu wa kada mbali mbali za kitaaluma na sio kwamba eti washairi ni watu wasiojuwa chochote katika taaluma nyenginezo.

Diwani hii ya Ndimi Zenye Ncha, ni Diwani ya kipekee inayojibu dhana ya kwamba Ushairi wa Kiswahili ni makhsusi kwa jamii ya Wanaume pekee na kuwarembelea mbali Wanawake wasijihusishe kabisa katika Tasnia hii, ukipitia katika ukurasa wa “YALIYOMO” utagundua majina yafuatayo, Sharifa Khamis Mussa, Sabrina Suleiman Mohammed, Fatma Salim Mohammed, Asha Abdulla Mussa, Rufea Makame Bakar, Bimkubwa Mfaume Mohammed, Mwanacha Mohamed Omar, Bimkubwa Juma Said, Tatu juma Maalim, Hadija Ali Mohamed, Khadija Rashid Hossein, Saumu Miraj Yunus, Mayasa Khamis Haji na Thuwaiba Abdulla Omar, ukisoma orodha hio, utakuta idadi ya wanawake 14 kati ya washiriki 34 walioifanya Diwani hii ikamilike, idadi hio ndefu ya wanawake inajenga dhana ya kwamba kumbe Ushairi wa Kiswahili ni kwa jinsia zote, na sio kwamba ni Tasnia ya wanaume pekee.

Ukirudia tena kusoma kurasa za “YALIYOMO”, pasi shaka utakubaliana nami kwamba kumbe, Tasnia ya Ushairi inaweza kuwaunganisha watu walio katika sehemu tafauti ya dunia na kuwaweka katika sehemu moja, “Diwani ya Ndimi Zenye Ncha” inathibitisha hilo, kwani waandishi wa diwani hii kuna watu wanaoishi mitaa mbali mbali ya Unguja na Pemba, kuna washiriki kutoka Mikoa tafauti, ikiwemo Arusha na Dar Es Salaam lakini ajabu zaidi kuna mpaka mshairi ambaye anaishi jijini Bonn, Ujarumani, hii yote inaonyesha kwambaTasnia ya Ushairi ina nguvu kubwa katika mambo mengi ya kijamaa ikiwemo kuwaleta watu pamoja.

Ukiwa utaisoma diwani hii hata kijuu juu tu, basi hutaacha kuona jinsi Diwani ya Ndimi Zenye Ncha inavyogusa nyanja mbali mbali katika jamii, ukifungua ukurasa wa 7 tu utakutana na shairi liitwalo “MWANANGU”, ni shairi ambalo mzazi anavyompa nasaha mwanawe juu ya Ulimwengu na Walimwengu 

“Nisemayo uyashike, tena uyazingatie,

Usije ubabaike, mwishowe vikuzidie,

Watu walimwengu wake, kupambambanua ujue,

Nakuusia mwanangu, dunia na walimwengu”

Nukuu hii ya ubeti wa kwanza shairi hili, inakata kile kidomo domo cha waja wa zama hizi, kudhani kwamba ushairi wa Kiswahili una ujumbe wa kimapenzi pekee na kuiaminisha hadhira kwamba, kumbe Ushairi unatoa na kufikisha elimu kwa Nyanja zote kupitia midundo yake maalum.

Nasaha zangu kwa jamii ya Kizanzibari na Tanzania wanunuwe Diwani ya Ndimi Zenye Ncha kwa shilingi elfu kumi za Kitanzania (Tsh. 10,000/-) ili wapate ladha yake, humu muna ladha tamu iliyofinyangwa finyangwa na waandishi walioandika Diwani hii, kwani ndimi za Washairi hawa zimenena yote yatakayo kunenwa, ambayo kwa Tasnia nyenginezo hayawezi kunenwa, lakini kwa Ushairi hunenwa yakaneneka, na kumfanya anenezwaye aelewe na afahamu.

Wahi mapema usingoje kuhadithiwa, nakala ni chache sana.

Kwa mawasiliano piga namba 0774645030/0776820608.


Ahsanteni sana

Ali Mohammed Ali (Almar)

Mwandishi na Mtunzi wa Kazi za Fasihi

Mshiriki wa Diwani ya Ndimi Zenye Ncha

Mshindi wa Nne wa Tuzo ya Ushairi ya TUEHU 2019

Kisauni – Unguja

Zanzibar

11/10/2020

Saturday, January 25, 2020

HUSDA NASHEED

HUSDA

1. Macho yangu nayalenga, kwako wewe mwanadamu
Unokwenda kwa waganga, mwengine kumdhulumu
Tena mipango wapanga, hata kwa kumwaga damu

2. Husda imejikita, imo kwenye yako damu
Ya kheri yanakupita, wakumbatia haramu
Kulala wasitasita, wakesha kwenye mizimu

3. Lengo yeye vimtoke, kuwa navyo huna hamu
Watoto na mali zake, vyote unavihujumu
Utu na thamani yake, kwake iwe ni hatamu

4. Mwanaadamu zinduka, husda siyo muhimu
Tujiepushe haraka, tabia hii ni sumu
Akhera tutapofika, Kuna moto Jahanamu


Kiitikio
Husdaa... Husdaa... Husdaaa... Kwetu hatari
Husdaa... Husdaaa.... Husdaaa.. tujihadhari

Saturday, October 12, 2019

MJUE MFUNGWA HURU

MJUE OTHMAN AME HAMZA (MFUNGWA HURU) KUPITIA MAHOJIANO HAYA YALIYOFANYIKA KATIKA KUNDI LA WASAP LIITWALO MALENGA CHIPUKIZI (12/9/2019)

ABU HAYTHAM: πŸŽ™πŸŽ™πŸŽ™
Bwana Othman, karibu katika studio zetu za Malenga Chipukizi, karibu ukaribie

Mfungwa huru: 
Shukran nimekaribia

ABU HAYTHAM: Assalaamu alaykum alhabeeb, wajionaje na hali?

Mfungwa huru: Waalaykum salam, Hali yangu iko vyema alhamdulillah

ABU HAYTHAM: Mkeka upo, kama wahisi kiti hakikupi utulivu tuketi mkekani

Mfungwa huru: πŸ˜‚πŸ€£ panatosha kitini

ABU HAYTHAM: Maa shaa Allaah! Nadhani wana malenga wanakufuatilia kwa karibu kabisa. Hebu jitambulshe walau kwa muhtasari

Mfungwa huru: Naam, Jina langu ni Othman Ame Hamza, kwa jina la lakabu ni Mfungwa huru... Mzaliwa wa Donge, Unguja Zanzibar na ndipo makaazi yangu kwa sasa

ABU HAYTHAM: Aywaa, labda tuanze hapo kwenye lakabu ya "Mfungwa Huru". Ilikuwaje na ufungwa wa uhuru alhabeeb?

Mfungwa huru: Ah! Jina hili linatokana na shairi langu ambalo binafsi nililipenda sana, mwanzo wa shairi hilo nililipa anuani "wafungwa huru" lakini nikahisi nikitumia nafsi ya umoja litakaa vizuri... Kwa hiyo jina linatoka hapo, ilikuwa kama ilhamu tu

ABU HAYTHAM: Marhabaa, hili ni shairi lako la kwanza au la ngapi kama unakumbuka?

Mfungwa huru: Kiukweli siyo la kwanza, nilishawahi kuandika mashairi matano kabla ya hili,

ABU HAYTHAM: Safi sana, tuhame huku kwanza tutarudi baaden.

Kwanza kwa niaba ya wafuatiliaji nikupongeze sana kwa kuanzisha ukumbi huu. Mola akulipe kila la kheri

Mfungwa huru: Amiin, kwa sote insha Allah

ABU HAYTHAM: Na natazama tarehe, yaonesha mwezi ujao ukumbi huu utakuwa unatimiza miaka miwili kamili.

Labda ulisukumwa na nini na ulifikiria nini hadi ukaanzisha ukumbi huu adhimu?

Mfungwa huru: Ahaa! Historia ya ukumbi huu ni kubwa sana,
Tulipokuwa chuoni SUZA kulikuwa na kundi la NKURUMAH DEGREE EDUCATION sisi wapenzi wa mashairi kipindi hicho tulikuwa tunatuma kazi zetu huko, Ila baadhi ya watu hawakufurahishwa, hapo tukashauriana Mimi na bwana Abdillah Mohammed (Mcheza kwao) tuanzishe kundi la mashairi kwa ajili ya darasa letu , tulikubaliana tukaanzisha kwa ajili ya NKURUMAH tu pekee kwa wakati huo.Baadae tukalenga kwa ajili ya Wanafunzi wa Zanzibar tu hata kama wanasoma nnje ya Zanzibar, lakini Mambo yaliponoga na kupata watu wengi zaidi kwa sasa ni kundi lenye malengo makubwa zaidi ya hayo ya awali, naweza kusema kikundi kimekuwa

ABU HAYTHAM: Naam, Ni kweli, sasa kimekusanya wengi wasomao na wafundishao

Mfungwa huru: πŸ€£πŸ˜‚πŸ˜‚naam

ABU HAYTHAM: Unajiskiaje unapoona huu ukuaji wa kikundi?

Mfungwa huru: Napata faraja sana, na hupenda watu wakiingia humu hata kama hawatungi basi wasitoke, muhimu ni kuwekeana heshima tu baina yetu, pia tuwe na dira na malengo yanayofanana

ABU HAYTHAM: Hakika!
Bwana Othman nakufahamu kama mshairi, bila kujali kiwango chako na vyovyote ujiitavyo.
Wafuatiliaji wanapenda kujua, je katika familia yenu kuna asili ya ushairi? Yaani kuna mtu yeyote katika familia alikuwa ni mshairi?

Mfungwa huru: Dah! Sina uhakika na sikumbuki kama nyumbani palitokea mshairi, Ila Nina mjomba ambaye anatunga tenzi hasa za sherehe za maulidi, na za kichama

ABU HAYTHAM: Alaa, unataka kusema kuwa mjomba ni moja ya watu waliokuvuta ushairini?

Mfungwa huru: Nathubutu kusema hivyo,

ABU HAYTHAM: Au kuna wakongwe wengine waliokuvuta?

Mfungwa huru: Unajuwa Mimi ni mpenzi wa mashairi tangu nikiwa mdogo bila kujijuwa, nilipenda sana kusoma qaswida nilipokuwa madrasa, Sasa tukipata mialiko baadhi ya madrasa pia huzisikia tenzi za mjomba zikaghaniwa, nilikuwa napenda sana, Na kipindi hicho ilikuwa sijui chochote kuhusu ushairi,

ABU HAYTHAM: Vyema sana, naweza sema ushairi umeshapenya damuni mwako.

Pengine twataka kujua, shairi la kwanza ulilitunga lini na linakwenda na maudhui gani?

Mfungwa huru: Swali hili linanipa kigugumizi kidogo,
Ila Shairi langu la kwanza nililitunga nikiwa kidato Cha nne, lilihusu elimu (sikulihifadhi kwa njia yoyote)

ABU HAYTHAM: Oh! Pole sana

Mfungwa huru: Ahsante

ABU HAYTHAM: Napata nyepesinyepesi kuwa una diwani ipo sokoni, hili lina ukweli wowote?

Mfungwa huru: Diwani zipo, alhamdulillah,

ABU HAYTHAM: Kwani zipo nyingi?

Mfungwa huru: Zipo 2,

ABU HAYTHAM: Sawa, labda tujaalie majina na zinauzwaje?

Mfungwa huru: Diwani ya kwanza nilishirikiana na Washairi watatu Binti bogoyo, Mcheza kwao, na mwalimu NAM ambayo inaitwa MALENGA WA ZENJI Nna ya pili ambayo imetushirikisha Wanafunzi wengi kutoka SUZA inaitwa KILINGE CHA UKOMBOZI, zote hizi zinauzwa kwa shilingi 8000 tu za Kitanzania.

ABU HAYTHAM: Maa shaallah. Othman, katika vitu ambavyo husemwa kuhusu uandishi hasa wa mashairi ni kwamba washairi ni watu duni na pia ushairi ni wa wazee. We walionaje hili, au hujawahi kukutana nalo?

Mfungwa huru: Kuhusu ushairi ni wa wazee sijawahi kukutana nalo, Ila kuhusu Washairi ni watu duni hasa kimaisha tayari nimeshakutana nalo

ABU HAYTHAM: Umesema kuwa washairi ni watu duni sana hasa kimaisha, na umekiri kukutana na jambo hili. Umekutana nalo wapi?

Mfungwa huru: Kwanza nakiri kwa kulisikia midomoni mwa watu wengi, haswa washairi wenyewe... Pia Kuna ushahidi nachelea kuutoa, lakini wacha nikate jongoo kwa meno... Mfano mshairi Haji Gora ukifuatilia hadhi yake kimashairi na maisha yake ni vitu viwili tafauti na sio huyo tu ata Washairi wengine 

ABU HAYTHAM: Alaa

Mfungwa huru: Naam

ABU HAYTHAM: Ni kweli yasikitisha, na mfano wako wasemwa na wengi. Labda wewe kama mshairi unayekuja kwa kasi, unadhani hili litapunguaje hadi tuseme limekwisha?

Mfungwa huru: Dah! Umenikweza Sana, Ila kupunguwa kwake kwanza washairi tuwe kitu kimoja, tuungane mkono katika kazi zetu ambazo tunazifanya, pia kutetea maslahi yetu kwa pamoja... Kwa namna yoyote ile hata kama kwa kuanzisha jumuiya na vyama vyenye kusimamia washairi

ABU HAYTHAM: Nimekupata sana...

ABU HAYTHAM: Kila msanii huwa ana kiigizo, wazungu wanasema Role Model. Siamini kama wewe huna, tujaalie tumjue umuigaye au utamaniye kuwa kama


Mfungwa huru: Natamani kuwa Kama wengi tu, Mimi washiri wengi natamani kuwa Kama wao. Kuhusu nimuigae, nawaiga wengi pia

ABU HAYTHAM:
Wakati unaanza ushairi, lazima kuna washairi wakubwa wa kale ulikuwa ukiwapenda au hata sasa ujiendelezavyo kwa kusoma kazi zao unakiri ukongwe wao na ubobevu fanini.

Usitukatili, tutajie ili pengine nasi tujikongojao tunaweza kufukua kazi zao na kustaladhi kama wewe. Sogea karibu ya kipaza sauti, naona sauti yako imekuwa hafifuπŸŽ™

Mfungwa huru: πŸ€£πŸ˜‚sawa, Kama nlivyosema awali kuwa nlikuwa naupenda ushairi tangu zamani lakini sikujuwa nini hasa ushairi, nilipokuwa kidato Cha tatu baada kusoma vitabu vya Malenga Wapya na Wasaka Tonge vilinivutia sana, naweza kusema wenye vitabu hivi kwangu ulikuwa ni mfano wa kuwaiga, lakini kila nilipojifunza nilikutana na wengi zaidi ya hao,

 ABU HAYTHAM: Sawa sawa...

Labda tuambie lini hasa uliona kuwa ushairi unaanza kukukubali na kwa hilo ukaazimia kutouacha?

Mfungwa huru: Baada ya Kutunga Shairi la "Mfungwa huru" mwaka 2017 Kama mwezi wa 9 hivi,

ABU HAYTHAM: Baada ya kipindi tutakuomba utuoneshe ili nasi tuhamasike, tuelimike na tuburudike

Mfungwa huru: Kwa wale wenye nakala za Malenga wa Zenji Shairi linapatikana humo, lakini pia nitalituma, usijali

ABU HAYTHAM: Naomba kwa ridhaa yako, niruhusi maswali mawili kutoka kwa wasikilizaji
Kabla sijamaliza kwa maswali mawili ya mwisho

Mfungwa huru: Wasikilizaji na watazamaji karibuni

BONGO TATA: Mzee mimi kwanza ameoa na kama ameoa kivip anweza kudhibiti mda wa ndoa na sanaa

Mfungwa huru: Jawabu ni fupi tu,,, bado sijaoa

ABU HAYTHAM: Tunashukuru, maana yake na swali la pili limekufa kifo cha kawaida...

ABU HAYTHAM: Nafasi ya mwisho kwa mfuatiliaji mwingine...

ABU HAYTHAM:Tumalize, kwa kukushukuru sana kwa muda wako.
Tunakuomba tu utustahmilie na utuwie radhi. Tupigie picha shairi lako la Mfungwa Huru kutoka katika diwani tajwa
 Na utueleze kuwa diwani yako inapatikanaje kwa mwenye kuihitaji

Mfungwa huru: Kwa Sasa hapa nilipo sina nakala, ipo sehemu nyengine, Ila nitatumia njia nyengine mtalipata
 Diwani kwa Sasa kwangu  kopi zimemaliza, labda kwa Mcheza kwao au binti bogoyo Kama zipo,

ABU HAYTHAM: Tafadhali Bwana Othman kwa muda wako na ninakushukuru sana, malizia kahawa yako na nikutakie usiku mwema

Mfungwa huru: Ahsante, shukrani na wewe pia

Sunday, September 29, 2019

Kilinge cha Ukombozi

Kilinge Cha Ukombozi ni kitabu cha Mashairi kilichotungwa na washairi chipukizi pia wakiwa ni Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA). Mawazo ya kuandikwa kwa Kitabu hiki yametoka kwa uongozi wa CHAWAKAMA-SUZA  wa mwaka 2018/2019 ukiwa chini ya mwenye kiti Abdillah Mohammed Kassim (Mcheza kwao). Wazo Hilo liliwafikiwa na kuratibiwa kwa ajili ya kuazisha shindano  mbalo lingewezesha kupatikana kwa Mashairi hayo. Mashairi hayo yalikusanywa na mhariri mkuu ndg. Othman Ame Hamza (Mfungwa huru) kwa ajili ya kupata washindi. Kwa kuwa washiriki walikuwa wengi washairi 25 wa mwanzo  walibahatika kuingizwa pamoja na viongozi 10 waliotunga Mashairi yao hapo awali. Kitabu hiki  kimehaririwa kwa ustadi na umahiri mkubwa na Dkt. Omar Salum Mohamed na kuchapishwa kwa mara  ya kwanza  na Mwimbe Priters iliyopo Bagamoyo mwaka 2019. Kuandikwa kwa kitabu hiki kumetokana na sababu nyingi.
Kwanza, kuendeleza na kukuza lugha ya Kiswahili,
Pili, kuendeleza na kukuza vipaji vya washairi hasa chipukizi
Tatu,kuchochea uwandishi wa kazi za kifasihi hasa kwa upande wa Zanzibar.
Nne kuhifadhi na kulinda utamaduni wa Mswahili.

Friday, May 31, 2019

SHAIRI: LAKINI?

*_LAKINI!_*

Sauti yangu napaza, isikike hadharani
Mema nikiyatangaza, na mabaya kubaini
Lakini! sitaki kwaza, Mfungwa si kifungoni


Barabara zipo nyingi, mijini na vijijini
Hili jambo silipigi, jitihada nabaini
Lakini! ajali nyingi, twapinduka mashimoni


Maji Safi na salama, twayapata majumbani
Bomba zisambaa vyema, zimeungwa kwa makini
Lakini! metuandama, tulipe mwisho mwezini


Elimu inapepea, imekuwa afueni
Watoto wajisomea, bure tena kwa amani
Lakini! najionea, mwalimu hali ni duni


_*Litaendelea*_

_*Lakini! Sijui lini!*_


_*Mfungwa huru*_
othame10@gmail.com

Sunday, April 14, 2019

MFUNGWA HURU

_*NUSU ZUZU,NUSU ZEZETA*_

Akili nusu zezeta, nusu imekuwa zuzu, umeizuzua
Mwili umenizorota, mwembamba kama kauzu, umejikondea
Moyo unanitukuta, tuu! tuu! unajuzu, umeuonea


Miguu hafurukuta, imeingia kibibi, haina hisia
Tumbo linanisokota, umeisha ujanabi, umeshakimbia
Leo hii wanisuta, huniti tena hababi, yako kutumia


Huba kwako limekata, thamani 'mepukutika, ulonipatia
Kuna jambo ulifata, leo umenifutuka, hukua na nia
Ipo siku nitapata, mrembo kukufunika, alietimia


Uchungu umenipata, hadi haya kuandika, jua naumia
Shauri tulolikata, kuwa sote tutafika, hadi kwenye ndoa
Ni ruya yenye utata, na zuzu nimezuzuka, bora kujifia


Funzo nimeshalipata, kwako nilifanya kosa, sitalirejea
Nenda na mimi 'tapata, mzuri asie visa, na mbaya tabia
Amba mimi ni zezeta, na zuzu mtoa pesa, niko safi nia



_*Othman Ame Hamza*_
*_Mfungwa huru_*
0776820608
othame10@gmail.com

Friday, December 28, 2018

_*KWA NINI YEYE?*_

Utungo nauandika, ituondoke jefule
Papara napaparika, kutoa zangu kelele
Moyoni naungulika, kwa kuwapo hili ndwele
Fikiri yangu kauli,  kisha toa muamuzi


Kwa nini yanamfika, mazito pasi sumile?
Kigori adhalilika, kwenye ndoa awe pale
Huku mkifurahika, shangwe na vigelegele
Fikiri yangu kauli, kisha toa muamuzi


Ndoani mwampeleka, hana nyuma wala mbele
Umri haujafika, kumudu vishindo vile
Baba limesawijika, kwichi! kwichi! makelele
Fikiri yangu kauli, kisha toa muamuzi


Kauli mnatamka, eti sababu wavyele
Wajukuu mnataka, kutoka kwa wanakele
Wallahi mmepotoka, upotofu toka kale
Fikiri yangu kauli, kisha toa muamuzi


Haki kwake inavuka, aishi ja msukule
Vidato alivitaka, aweze kusonga mbele
Ila wapi! patashika, hana nguvu ni m-bole
Fikiri yangu kauli, kisha toa muamuzi


Tusubiri kupevuka, tulichume kwa upole
Tunda lililitukuka, hadhi itabaki pale
Changa haiba hushuka, madhara kimaumbile
Fikiri yangu kauli, kisha toa muamuzi


Beti saba zimefika, nishaigonga kengele
Wenye Sikio pulika, macho yatoe miale
Tan-bihi nimeweka, yasijirudie yale
Fikiri yangu kauli, kisha toa maamuzi


_*Jina la mtunzi: Othman Ame Hamza (Mfungwa huru)*_

_*Mzaliwa wa Donge, Unguja Zanzibar*_

☎0776820608

Barua-pepe othame10@gmail.com