_*KWA NINI YEYE?*_
Utungo nauandika, ituondoke jefule
Papara napaparika, kutoa zangu kelele
Moyoni naungulika, kwa kuwapo hili ndwele
Fikiri yangu kauli, kisha toa muamuzi
Kwa nini yanamfika, mazito pasi sumile?
Kigori adhalilika, kwenye ndoa awe pale
Huku mkifurahika, shangwe na vigelegele
Fikiri yangu kauli, kisha toa muamuzi
Ndoani mwampeleka, hana nyuma wala mbele
Umri haujafika, kumudu vishindo vile
Baba limesawijika, kwichi! kwichi! makelele
Fikiri yangu kauli, kisha toa muamuzi
Kauli mnatamka, eti sababu wavyele
Wajukuu mnataka, kutoka kwa wanakele
Wallahi mmepotoka, upotofu toka kale
Fikiri yangu kauli, kisha toa muamuzi
Haki kwake inavuka, aishi ja msukule
Vidato alivitaka, aweze kusonga mbele
Ila wapi! patashika, hana nguvu ni m-bole
Fikiri yangu kauli, kisha toa muamuzi
Tusubiri kupevuka, tulichume kwa upole
Tunda lililitukuka, hadhi itabaki pale
Changa haiba hushuka, madhara kimaumbile
Fikiri yangu kauli, kisha toa muamuzi
Beti saba zimefika, nishaigonga kengele
Wenye Sikio pulika, macho yatoe miale
Tan-bihi nimeweka, yasijirudie yale
Fikiri yangu kauli, kisha toa maamuzi
_*Jina la mtunzi: Othman Ame Hamza (Mfungwa huru)*_
_*Mzaliwa wa Donge, Unguja Zanzibar*_
☎0776820608
Barua-pepe othame10@gmail.com
No comments:
Post a Comment