Monday, March 5, 2018

WASIA WA BABU

Babu kabla ya kufa, usia kunipatia.
Kwamba dunia maafa, nikae kuzingatia.
Akanipa zake sifa, Nzuri na mbaya pia.
Usia wake daima, kamwe sitausahau.


Duniani yapo mengi, alianza nihusia.
Aliyapaka na rangi, mazuri alonambia.
Ila jambo la msingi, niweze yazingatia.
Usia wake daima, kamwe sitausahau.


Pia alinihusia, dunia ina anasa.
Usije kuzipania, sikia ninakuasa.
Wengi walishapotea, kisingizio siasa.
Usia wake daima, kamwe sitausahau.


Sikio alinishika, ataka nizingatie.
Kukaa na Kila rika, wala nisizibague.
Ila pazuri kushika,  penye kwendana na mie.
Usia wake daima, kamwe sitausahau.


Aliingiwa na hari, nikawa nampepea.
Akanza tahayari, na sana kunihofia.
Mithili maji bahari, machozi aliyatoa.
Usia wake daima, kamwe sitausahau.


Alinihusia mengi, niepuke marafiki.
Wale wavutaji bangi, na wanao kunywa arki.
Hata wale mashangingi, bure watakuhilaki.
Usia wake daima, kamwe sitausahau.


Mwisho alinihusia, dunia ni kama njia.
Kaa na waja kwa nia, njema isiyoudhia.
Shida wakikuletea, waweza wasaidia.
Usia wake daima, kamwe sitausahau.


_*By ochu*_

_*Mfungwa huru*_







NAKIREJEA KIMEO

Naja mbele ya umati, naandika kusudio.
Naililia bahati, niko hoi mbiombio.
Taabani mahatuti, zinipungue hashuo.
Sitoacha              m-bachao, nakirejea kimeo.


Dharau zimeniponza, kimeo kukifutuka.
Na sasa nimejifunza, kimeo kina baraka.
Hizi kubwa  zaumiza, zaunguza ukishika.
Sitoacha m-bachao, nakirejea kimeo.


Sitoacha m-bachao, nakirejea kimeo.
Simu kubwa zao hao, wakubwa wenye na vyao.
Au pia mabishoo, wanouza sura zao.
Sitoacha m-bachao, nakirejea kimeo.


Bora kimeo cha jadi, tabu kwake sijapata.
Chaji natumia hadi, Masiku bila utata.
Nikichaji pasi kedi, kinajaa fastafasta.
Sitoacha m-bachao, nakirejea kimeo.


Kubwa zina mambo mengi, simu hizi za kisasa.
Utachaji mara nyingi, siku moja mara tisa.
Matumizi siyapingi, kama jicho ukipwesa.
Sitoacha m-bachao, nakirejea kimeo.


Yanitia mashakani,  simu ya androidi.
Simati foni si shani, mobaili ufisadi.
Kimeo kimfukoni, si kimoto kibaridi.
Sitoacha m-bachao, nakirejea kimeo.


Simu kubwa kuilinda, gadi inahitajia.
Hushuka Mara hupanda, mnara unasumbua.
Ikidondoka varanda, siyako nakuambia.
Sitoacha m-bachao, nakirejea kimeo.


Nakirejea kimeo, simatifoni yatesa.
Haya mambo ya kileo, bora niwe nayakosa.
Kila usiku uchao, uwe mpya ukurasa.
Sitoacha m-bachao, nakirejea kimeo.


Beti tisa zinatosha, nakirejea kimeo.
Hizi kubwa zakondesha, kimeo chanipa ngao.
Kimeo kwangu bashasha, hakihitaji mafao.
Sitoacha m-bachao, nakirejea kimeo.


*_BY OCHU_*
*_mfungwa huru_*

No comments:

Post a Comment