Saturday, March 10, 2018

***KIGENGE***

1)Huu wangu mtazamo, nionavyo nawambia. Hisia ziumoumo, nihisivyo nazitoa. eti ni mdogo kimo, na miaka mtazua. Kigenge kimetubana, ngama yatutoka nyuma.


2) Watasema siyajui, yaliotokea nyuma. waliuwa maadui, kigenge kikasimama. Ila sasa hakifai, kinatukondesha nyama. Kigenge kimetubana, wala hatufurukuti.


3) Kigenge hicho sikia, wizi wa kupindukia. shitaka ukifungua, hongo wanahitajia. Bangi unga huingia, bila ya kuwazuia. Kigenge kimetubana, ngama yatutoka nyuma.


4)Sikichukii kigenge, ila siwapendi watu. Wala sipendi kigenge, bali nawapenda watu. Wanaojali wanyonge, kuthamini wao utu. Kigenge kimetubana, wala hatufurukuti.


5) Kigenge kipo zamani, enzi zile za mababu. sasa hakina thamani, kimetutoka muhibu. Waongezeka wahuni, ukweli twapata tabu. Kigenge kimetubana, ngama yatutoka nyuma.


6) Kigenge mbona si shwari, kinahodhi mali zetu. sasa kikirikikiri, tunamwaga damu zete. Kwa bongo na ujasiri, kurejesha utu wetu. Kigenge kimetubana, wala hatufurukuti


7)Mwisho nanena kigenge, tukiroge uchawini. Gerezani tukifunge, kisitoke abadani. sote pamoja wanyonge, tutashinda kwa imani. Kigenge tukiondoe, wahuni wamalizike...



Mtunzi: Othman Ame Hamza.
Lakabu: Mfungwa huru [Free prisoner]
Mshairi wa Donge...
Tel:0776820608
HAKI ZOTE  ZIMEHIFADHIWA

No comments:

Post a Comment