Monday, March 12, 2018

TAMBIKO LA AFRIKA

Bara letu afrika, kubwa la pili dunia.
Likambiwa chakarika, mafao kujipatia.
Likapuuza hakika, sasa linajijutia.
Sisi wanaafrika, hili ndo tambiko letu.

Sisi wanaafrika, malofa yulokithiri.
Kwetu mejaa baraka, bado twaitwa fakiri.
Tatizo yote kufika, ujinga meshika ari.
Sisi wanaafrika, hili ndo tambiko letu.

Tukanaitwa kwa majina, nchi zinoendelea.
Kwa sifa tunajivuna, bara salama dunia.
Maendeleo hakuna, twabaki twadidimia.
Sisi wanaafrika, hili ndo tambiko letu.

Pia jina linotisha, bara dunia ya tatu.
Maradhi tunahuisha, kwa ongezeko la watu.
Ya Ebola hatarisha, ukimwi mejaa kwetu.
Sisi wanaafrika, hili ndo tambikoletu.

Sisemi kwa kulibeza, moyoni ninamachungu.
Iweje wao waweza, sisi tuwe nyuma tangu.
Au ndo tumebatizwa, tusiwe kama wazungu?.
Sisi wanaafrika, hili ndo tambiko letu.


 Mfungwa huru

No comments:

Post a Comment