MFUNGWA HURU
Naja kwenu kwa unyonge, kueleza yanosibu.
Mistari niipange, na vina vyastahabu.
Kibwagizo nikifunge, kwa neno lenye ajabu.
Mimi ni mfungwa huru, dunia ndio gereza.
Kua mwana utaona, niliambiwa zamani.
Usayaona mchana, utayaona gizani.
Dunia wanja wa lana, kweli sasa mebaini.
Mimi ni mfungwa huru, dunia ndio gereza.
Dudia sasa yatisha, vitendovye hayawani.
Mambo yanoatilisha, hayo mejaa pomoni.
Si kama namaanisha, kukosoa kudurani.
Mimi ni mfungwa huru, dunia ndio gereza.
Duniani kuna watu, waliotaalamika.
Wanotengeza mitutu, na mabomu kadhalika.
Ili kuulia watu, ulinzi pia kuweka.
Mimi ni mfungwa huru, dunia ndio gereza.
Eti ni maendeleo, kuigawanya mipaka.
Ya dunia midenguo, isijekukuachika.
Utaitafuta ngao, ushindwe pakwenda shika.
Mimi ni mfungwa huru, dunia ndio gereza.
Dunia kama kijiji, watu wamekigeuza.
Sio nchi wala miji, wote wamejitandaza.
Sio tu kupiga maji, neno chafu kucharaza.
Mimi ni mfungwa huru, dunia ndio gereza.
Yale yanonishangaza, kufumbua mboni zangu.
Nikiona chapendeza, kumbe pia ni kichungu.
Mapenzi yaniburuza, kweli hii jela chungu.
Mimi ni mfungwa huru, dunia ndio gereza.
Ukingalia kwa kina, utaona yapendeza.
Mapambo kila aina yaliyojilimbikiza.
Usiku kama mchana, kweli hii miujiza.
Mimi ni mfungwa huru, dunia ndio gereza.
Kila nikisonga mbele, nafsi inanitetema.
Kutoa zangu kelele, moyoni wanisakama.
Wanataka niwe kule, enzi za baba na mama.
Mimi ni mfungwa huru, dunia ndio gereza.
Nakuomba uzinduke, mwana wa kidigitali.
Hali yangu ikumbuke, ilivyokuwa dhalili.
Vituko anasa zake, jela hii ni katili.
Mimi ni mfungwa huru, dunia ndio gereza.
*_by mfungwa huru_*
No comments:
Post a Comment