Saturday, March 10, 2018

BADO HAMJABWABWAJA

Kila muda vikundini, midomoni kututia.
Tushuke zetu thamani, hili tumeshitukia.
Kusengenya namba wani, kuropokwa mezoea.
Bado hamjabwabwaja, zidisheni nawambia.

Si mipasho ikhiwani, ujumbe kwenu twatoa.
Tumechoka kwa yakini, ila tunavumilia.
Maji kitia katani, yakogee sije poa
Bado hamjabwabwaja, zidisheni nawambia.

Tumetia akilini, maneno munorongoa.
Ila siyapi imani, kwetu yanatuchefua.
Wanazusha tafrani, ugomvi kuuibua.
Bado hamjabwabwaja, zidisheni nawambia.

Wazidi chochea kuni, moto uzidi kolea.
Kuyazua yetu kwani, hili halijasumbua.
Tunang'ara izirani, kama miale ya jua.
Bado hamjabwabwaja, zidisheni nawambia.

Mwabwabwaja hadharani, thamani zetu kutoa.
Kuwambia wafulani, ndiko munaabudia.
Hatushughuliki kwani, yetu yanatuendea.
Bado hamjabwabwaja, zidisheni nawambia.

Beti sita uwanjani, zitoshe kuwaambia.
Kubwabwaja toshekeni, muda wenu wapotea.
Kutusema vikundini, kwikwi zitawapalia.
Bado hamjabwabwaja, zidisheni nawambia.



*_By ochu_*

*_Mfungwa huru_*

No comments:

Post a Comment