Sunday, September 9, 2018

NAMTAFUTA SUNGURA

Naanza kwa shukurani, kumshukuru jalia.
Mola asie wa thani, peke twamuabudia.
Furaha na mitihani, yote ametuambia.
Namtafuta sungura, wangu amenikimbia.


Nilimfuga nyumbani, uzio kumzingia.
Nikampa na majani, mboga akafakamia.
Sasa yupo vijiani, mimi amenikimbia.
Namtafuta sungura, wangu amenikimbia.


Siku za nyuma utani, sungura kanifaniyia.
Ikawa purukushani, kumbe amedhamiria.
Anapenya uzioni, kisha namfukuzia.
Namtafuta sungura, wangu amenikimbia.


Sungura wangu wa shani, ni mweupe asili.
Musijefanya utani, hapa nilipo nalia.
Huu kwangu mtihani, kweli umenishukia.
Namtafuta sungura, wangu amenikimbia.


Jama nisaidiani, mikononi kumtia.
Waunguja ungujani, ndipo alipokimbia.
Huwenda yu baharini, pemba anaelekea.
Namtafuta sungura, wangu amenikimbia.


Mcheza kwao yakini, ndugu yangu naumia.
Bogoyo baba mwandani, mwanao wanisikia.
Ngozi katibu makini, kwako ninakimbilia.
Namtafuta sungura, wangu amenikimbia.


Babu la nungwi ugani, ticha hassani sawia.
Suhusu alwatani, hima kunisaidia.
Mwezenu nitaabani, sungura namlilia.
Namtafuta sungura, wangu amenikimbia.


Sauti ngeni mbugani, ya wanyonge fikiria.
Ndiguyo nipo tabuni, kwikwi zinanipalia.
Sungura kawa muhuni, kashindwa kunisikia.
Namtafuta sungura, wangu amenikimbia.


Ubeti huu nadhani, ni wa mwisho kufungia.
Nimeiranda Chumbuni, sungura sejionea.
Mitaa ilojirani, sina budi kuingia.
Namtafuta sungura, wangu amenikimbia.



*_Mtunzi :Othman Ame Hamza (lakabu :mfungwa huru)_*
_*Makaazi: Chumbuni*_

☎0776820608
Barua-pepe:othame10@gmai.com

No comments:

Post a Comment