Saturday, March 3, 2018

Mashairi

1)SILAZIMISHI

Sitalazimisha katu, jembamba likawa nene.
Sitakuwa mtukutu, ukaidi niufane.
Tautunza wangu utu, hata nyinyi mnikane.
Cha kwangu hakiwi chako, mola ndie mpangaji.


Sitokivaa kiatu, pia huku kinibane.
Silazimishi papatu, miguuni kinichaane.
Siutaki ukurutu, nyayo jasho ziroane.
Cha kwangu hakiwi chako, mola ndie mpangaji.


Siwi kama mbwa mwitu, m-babe nionekane.
Jamii mambo na watu, sote tushirikiane.
Siwalazimishi katu, matusi msitukane.
Cha kwangu hakiwi chako, mola ndie mpangaji.


Mimi mtu kama watu, heshima tuwekeane.
Sitalazimisha katu, mimi nawe tufanane.
Katuumba mola wetu, ili tusaidiane.
Cha kwangu hakiwi chako, mola ndie mpangaji.


By ochu

Mfungwa huru






2)WANATAMANI NIZIKWE

Dunia ni mtihani, na ina mengi maafa.
Inanitia huzuni, macho yamefanya nyufa.
Watu Kama mashetani, nyoyo zao si nadhifa.
Ipo siku nitakufa, nakuzikwa nitazikwa.


Kwa nini mnatamani?, nizikwe bado sijafa.
Au nimekosa nini?, nikashusha zenu sifa.
Yenu madonge rohoni, yatatibia kifafa.
Ipo siku nitakufa, nakuzikwa nitazikwa.


Asiyekosa ni Nani?, akawa ja malaika.
Inanitia huzuni, makosa kunilimbika.
Nitazikwa kaburini, siku yangu ikifika.
Ipo siku nitakufa, na kuzikwa nitazikwa.


Siijui siku gani, nukta saa na dakika.
Wala sina upinzani, duniani tatoweka.
Kinafiki buriani, machozi yatawatoka.
Ipo siku nitakufa, na kuzikwa nitazikwa.


Ala moja asilani, hazikai panga mbili.
Nitakufa pasi shani, wakati kafa rasuli.
Namuomba rahmani, nife huku nikiswali.
Ipo siku nitakufa, na kuzikwa nitazikwa.


Beti sita za huzuni, sitaki nifike mbali.
Kufa kikondoo kwani,  kiungwana nakubali.
Mito hwenda baharini, wanadamu kwa jalali.
Nanyi pia mtakufa, na kuzikwa mtazikwa.


_*Ochu*_

_*Mfungwa huru*_

No comments:

Post a Comment