DIWANI YA NDIMI ZENYE NCHA
Katika zama ambazo, watu zama hizo hudhani kwamba Ushairi wa Kiswahili ni Tasnia inayowahusu watu wa kale au kwa lugha nyepesi wazee, na kamwe hauna nafasi, faida wala hadhi kwa vijana wa sasa.
Ni katika zama ambazo, watu wa zama hizo wamegubikwa na fikra za kwamba Ushairi wa Kiswahili katu hauna nafasi kwa watu wenye elimu za madaraja ya juu, ni kazi ambayo hufanywa na watu wasio na elimu pekee.
Ni katika zama ambazo, watu wa zama hizo wamegubikwa na fikra za kwamba Ushairi wa Kiswahili ni Tasnia ambayo inapaswa kushughulikiwa na watu wa jinsia ya kiume pekee na kuwafanya wanawake kwamba hawana nafasi katika Tasnia hii.
Ni katika zama ambazo, watu wa zama hizo mawazo na fikra zao hudhani kwamba ushairi wa Kiswahili ni Tasnia ya kipuuzi ambayo hushughulikiwa na watu wasio na ujuzi wala kazi yoyote ya kitaalamu, bali ni watu wa maskani na vijiweni pekee ndio watu halali wa tasnia hii ya Ushairi.
Ni katika zama ambazo, watu wa zama hizo hudhani ya kwamba kazi kubwa ya Ushairi wa Kiswahili ni Tasnia inayoeleza ujumbe wa kimapenzi tu, hivyo wanaopaswa kushughulikia na watu fulani ambao fikra zao zaidi zimejikita katika mambo ya mapenzi na si vyenginevyo.
Ni katika zama ambazo, watu wa zama hizo hawana fikra za kwamba Ushairi wa Kiswahili unaweza kuwaunganisha watu wa maeneo mbali mbali ya nchi ya na kuwaweka sehemu moja.
Basi katika zama hizo hizo, ndipo mimi na wenzangu wa rika tafauti wakiwemo vijana wadogo, wazee, wanaume na wanawake wakaamuwa kukaa sako kwa bako, wakashikana mikono, wakaongozana hatuwa kwa hatuwa na kuamuwa kuziunganisha ndimi zao kwa pamoja zikawa ni “Ndimi Zenye Ncha”, tena zenye ncha kali, na kuamua kuziuwa na kuzizika fikra potofu na hasi za watu za zama waufikirio Ushairi tafauti na uhalisia wake.
Diwani ya Ndimi Zenye Ncha ni juhudi zetu Wasanii 34, ambao nia na dhamira ni kufikisha ujumbe kwa jamii kupitia Tasnia hii, walikaa pamoja, wakatafakari na kuamua kwa pamoja kutoa Diwani hii, kwa minajili ya kuvirithisha vizazi vilivyopo katika zama hizi na vile vya zama zijavyo Tasnia hii inayosemwa ndio Tasnia kongwe katika Kazi za Fasihi, huku wakikubaliana na msemo usemao “Nchi isio thamini Ushairi wake, basi nchi hio haina urithi” na wengine husema “Nchi isiyo na Washairi basi watu wa nchi hio ni sawa sawa na wafu”.
Washiriki wa Diwani hii ni watu wa umri na rika tafauti, humu kuna vijana wadogo ambao kama si maadili mema waliyoyapata kwa wazazi na jamii yao basi si hasha ukawakuta wakivaa milegezo na sarawili zilizochanwa chanwa mapajani na magotini, ili kudhihirisha ubarobaro na ujana wao, lakini kizuwizi cha maadili waliyokuzwa nayo ndicho kilichawafanya wasivae vivazi kama hivyo, pia wamo watu wa rika la kati kama langu sambamba na wazee wenye wajukuu, uwemo wao unaashiria kwamba kumbe Ushairi wa Kiswahili ni Tasnia ya watu wa rika zote.
Diwani hii pia ina washiriki wenye Elimu za Madaraja tafauti, kuna washiriki ambao hawakubahatika kupata elimu kabisa, kuna wenye elimu za wastani na kuna washiriki wenye elimu za ngazi ya Cheti, Stashahada, Shahada, shahada ya Uzamili na Shahada ya Uzamivu, tena wakiwemo wenye shahada za Uhasibu. Shahada za Uongozi, Shahada za Uwakili, Shahada za Nyukilia na Mionzi na nyenginezo, hii inaonesha dhahiri kwamba, kumbe Ushairi unawagusa watu wa kada mbali mbali za kitaaluma na sio kwamba eti washairi ni watu wasiojuwa chochote katika taaluma nyenginezo.
Diwani hii ya Ndimi Zenye Ncha, ni Diwani ya kipekee inayojibu dhana ya kwamba Ushairi wa Kiswahili ni makhsusi kwa jamii ya Wanaume pekee na kuwarembelea mbali Wanawake wasijihusishe kabisa katika Tasnia hii, ukipitia katika ukurasa wa “YALIYOMO” utagundua majina yafuatayo, Sharifa Khamis Mussa, Sabrina Suleiman Mohammed, Fatma Salim Mohammed, Asha Abdulla Mussa, Rufea Makame Bakar, Bimkubwa Mfaume Mohammed, Mwanacha Mohamed Omar, Bimkubwa Juma Said, Tatu juma Maalim, Hadija Ali Mohamed, Khadija Rashid Hossein, Saumu Miraj Yunus, Mayasa Khamis Haji na Thuwaiba Abdulla Omar, ukisoma orodha hio, utakuta idadi ya wanawake 14 kati ya washiriki 34 walioifanya Diwani hii ikamilike, idadi hio ndefu ya wanawake inajenga dhana ya kwamba kumbe Ushairi wa Kiswahili ni kwa jinsia zote, na sio kwamba ni Tasnia ya wanaume pekee.
Ukirudia tena kusoma kurasa za “YALIYOMO”, pasi shaka utakubaliana nami kwamba kumbe, Tasnia ya Ushairi inaweza kuwaunganisha watu walio katika sehemu tafauti ya dunia na kuwaweka katika sehemu moja, “Diwani ya Ndimi Zenye Ncha” inathibitisha hilo, kwani waandishi wa diwani hii kuna watu wanaoishi mitaa mbali mbali ya Unguja na Pemba, kuna washiriki kutoka Mikoa tafauti, ikiwemo Arusha na Dar Es Salaam lakini ajabu zaidi kuna mpaka mshairi ambaye anaishi jijini Bonn, Ujarumani, hii yote inaonyesha kwambaTasnia ya Ushairi ina nguvu kubwa katika mambo mengi ya kijamaa ikiwemo kuwaleta watu pamoja.
Ukiwa utaisoma diwani hii hata kijuu juu tu, basi hutaacha kuona jinsi Diwani ya Ndimi Zenye Ncha inavyogusa nyanja mbali mbali katika jamii, ukifungua ukurasa wa 7 tu utakutana na shairi liitwalo “MWANANGU”, ni shairi ambalo mzazi anavyompa nasaha mwanawe juu ya Ulimwengu na Walimwengu
“Nisemayo uyashike, tena uyazingatie,
Usije ubabaike, mwishowe vikuzidie,
Watu walimwengu wake, kupambambanua ujue,
Nakuusia mwanangu, dunia na walimwengu”
Nukuu hii ya ubeti wa kwanza shairi hili, inakata kile kidomo domo cha waja wa zama hizi, kudhani kwamba ushairi wa Kiswahili una ujumbe wa kimapenzi pekee na kuiaminisha hadhira kwamba, kumbe Ushairi unatoa na kufikisha elimu kwa Nyanja zote kupitia midundo yake maalum.
Nasaha zangu kwa jamii ya Kizanzibari na Tanzania wanunuwe Diwani ya Ndimi Zenye Ncha kwa shilingi elfu kumi za Kitanzania (Tsh. 10,000/-) ili wapate ladha yake, humu muna ladha tamu iliyofinyangwa finyangwa na waandishi walioandika Diwani hii, kwani ndimi za Washairi hawa zimenena yote yatakayo kunenwa, ambayo kwa Tasnia nyenginezo hayawezi kunenwa, lakini kwa Ushairi hunenwa yakaneneka, na kumfanya anenezwaye aelewe na afahamu.
Wahi mapema usingoje kuhadithiwa, nakala ni chache sana.
Kwa mawasiliano piga namba 0774645030/0776820608.
Ahsanteni sana
Ali Mohammed Ali (Almar)
Mwandishi na Mtunzi wa Kazi za Fasihi
Mshiriki wa Diwani ya Ndimi Zenye Ncha
Mshindi wa Nne wa Tuzo ya Ushairi ya TUEHU 2019
Kisauni – Unguja
Zanzibar
11/10/2020